Matukio na shughuli.

Tupo Sawa Organization
Usawa Endelevu · Matukio, kampeni na shughuli zetu za kijamii.

SANAA YA TUPO SAWA
12 Aprili 2026, 00:00
SANAA YA TUPO SAWA
SANAA YA TUPO SAWA ni mradi ulioanzishwa na Taasisi ya Tupo Sawa Organization kwa lengo la kuwawezesha watu wenye ulemavu kiuchumi kupitia utoaji wa mafunzo ya ujuzi na stadi mbalimbali zitakazowafungulia fursa za kiuchumi na kuwawezesha kujitegemea.
Programu ya mafunzo ya mradi huu imegawanyika katika makundi makuu mawili:
MAFUNZO YA USHONAJI (TAILORING TRAINING) – Kuwapatia washiriki ujuzi wa kushona na ushonaji wa mavazi ambao utawasaidia kuanzisha biashara zao wenyewe na kujipatia kipato.
MAFUNZO YA KUTENGENEZA SABUNI ZA MAJI (LIQUID SOAP MAKING TRAINING) – Kuwajengea washiriki uwezo na ujuzi wa kutengeneza sabuni za maji kama njia ya kujipatia kipato na fursa ya kujiajiri.
Kupitia mradi huu, Taasisi ya Tupo Sawa Organization inalenga kukuza uwezeshaji wa watu wenye ulemavu kiuchumi, kujitegemea, usawa wa fursa na ushirikishwaji wao katika jamii.

MEZA YA UPENDO: TUKIKUTANA MEZANI, TUNAJENGA JAMII JUMUISHI.
14 Februari 2026, 00:00
MEZA YA UPENDO: KUHAMASISHA UJUMUISHWAJI, USAWA NA UWEZESHAJI WA JAMII
Tarehe 14 Februari 2026, Taasisi ya Tupo Sawa iliandaa hafla ya Meza ya Upendo (Dining with Love) jijini Dar es Salaam, iliyowakutanisha watu wenye ulemavu, wazazi na walezi wa watoto wenye ulemavu, watoto yatima, viongozi wa Serikali pamoja na wanajamii mbalimbali katika meza moja. Mkutano huu ulikuwa ishara ya upendo, usawa, mshikamano na uthibitisho kwamba kila mmoja ana haki ya kuwa sehemu ya jamii bila kujali hali yake au uwezo wake.
Zaidi ya kushiriki chakula pamoja, washiriki walipata fursa ya kushiriki katika vipindi mbalimbali vya elimu na uhamasishaji vilivyolenga kuimarisha maendeleo ya mtu binafsi na jamii kwa ujumla. Mada zilizojadiliwa zilijumuisha:
Elimu ya Fedha: Kwa kushirikiana na UTT AMIS, washiriki walipata elimu kuhusu utamaduni wa kuweka akiba, mipango ya kifedha na fursa za uwekezaji kwa lengo la kuimarisha uwezo wao wa kujitegemea kiuchumi.
Kinga dhidi ya Matumizi ya Dawa za Kulevya: Washiriki walipata elimu kuhusu namna ya kuzuia matumizi ya dawa za kulevya na kulinda makundi yaliyo katika mazingira hatarishi, hususan watu wenye ulemavu.
Elimu ya Afya: Washiriki walielimishwa kuhusu umuhimu wa kuzingatia mtindo bora wa maisha, kujikinga na magonjwa na upatikanaji wa huduma muhimu za afya.
Milango ya Upendo: Kikao shirikishi kilichohamasisha upendo, huruma, mshikamano, kukubaliana na kuthaminiana, pamoja na uwajibikaji wa pamoja katika kuhakikisha hakuna mtu anayeachwa nyuma.
Kuimarisha Ushirikiano wa Kijamii: Hafla hii ilisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, viongozi wa jamii, mashirika ya kiraia na wadau mbalimbali katika kuendeleza ujumuishwaji wa jamii.
Meza ya Upendo ni sehemu ya dhamira pana ya Taasisi ya Tupo Sawa katika kukuza ujumuishwaji, usawa na uwezeshaji wa jamii. Kupitia programu kama hizi, taasisi inaendelea kuandaa majukwaa yanayowezesha watu kukutana, kujifunza, kubadilishana uzoefu na kushirikiana katika kujenga jamii ambayo kila mmoja anathaminiwa, anaheshimiwa na anapata fursa sawa za kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.

TAASISI YA TUPO SAWA YASHIRIKIANA NA AMO FOUNDATION KUWEZESHA WANAWAKE WENYE ULEMAVU KIUCHUMI
10 Aprili 2025, 00:00
Taasisi ya Tupo Sawa ikishirikiana na Amo Foundation iliendesha shughuli ya kutoa elimu na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu katika matumizi ya nishati safi ya kupikia. Tukio hili lililenga kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa upatikanaji wa nishati safi na salama ya kupikia kama sehemu ya kulinda afya, kuboresha mazingira ya maisha na kuimarisha fursa za kiuchumi.
Katika tukio hilo, msisitizo uliwekwa katika kuhakikisha kuwa wanawake na watu wenye ulemavu wanapata taarifa, elimu na fursa sawa za kunufaika na matumizi ya nishati safi ya kupikia. Aidha, jamii ilihamasishwa kutambua kuwa nishati safi ya kupikia inaweza kupunguza athari za kiafya zinazotokana na moshi wa kuni na mkaa, huku ikichangia kuboresha ustawi wa familia na kuongeza fursa za shughuli za kiuchumi.
Kupitia tukio hili, Tupo Sawa Organization iliendelea kusisitiza umuhimu wa ujumuishwaji katika mipango ya maendeleo na kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanashirikishwa kikamilifu katika upatikanaji wa huduma, teknolojia na fursa zinazoboresha maisha yao.
Tukio hili ni sehemu ya dhamira endelevu ya Tupo Sawa Organization ya kujenga jamii jumuishi, yenye afya bora, fursa sawa na uwezeshaji wa kiuchumi kwa wote.